JINSI YA KUPATA MTAJI NA KUANZA BIASHARA
Jacob Mushi
Entrepreneur
& Author
Arusha
Tanzania.
Habari za leo Rafiki Yangu
Nafurahi kuwepo pamoja na wewe ndani ya mwaka
huu mwingine. Leo nitumie nafasi hii ya kipekee kuandika kwako Heri Ya Mwaka
Mpya. Kuna mambo machache unatakiwa ujiulize Je eti ni kweli mwaka utakuwa mpya
kwako au ni zile kelele tu na hamasa? Una kitu gani unakitegemea kukipata cha
tofauti ndani ya mwaka huu 2017? Umeajiandaa vipi kukipata? Upo tayari kuwa
mpya ili upate hayo mambo mapya ya mwaka huu?
Tuachane
na hayo twende kwenye mada yetu ya leo. Nataka nianze na Makala hii kwa ajili
yako wewe unaedhani hujaanza biashara hadi leo kwasababu huna mtaji. Kwani
mwaka huu tena ukiendelea kulalamika huna mtaji ndio maana hujaanza biashara
tutakuacha mbali sana.
Maana
ya mtaji ni vitu vyote vya muhimu ambavyo vinahitajika kukusaidia katika
kuanzisha biashara yako. Kama ni hivyo basi wewe pia unaanza kuwa mtaji.
Capital
Is not only money (Mtaji sio Pesa Peke yake)
Kuna
vitu vingi sana ambavyo vimekuzunguka na unaweza kuanza kuvitumia kama mtaji wa
kukuzia biashara yako. Naelewa sio kila biashara unaweza kuanza bila pesa
kabisa lakini kama huna pesa na hujapata popote kwa kukopeshwa unafanyaje?
Utabaki kuendelea kulalamika umekosa mtaji? Kwanza ukishajua unataka nini au
unataka kufanya biashara gani ndio inakua rahisi Zaidi kujua utaanzaje kama ni
bila mtaji kabisa au kwa kiasi kidogo. Mtaji wa kwanza ulionao ni wewe
mwenyewe. Yaani wewe ndie mfanyakazi wako wa kwanza unatakiwa ujue kujitumia
ili uzalishe pesa. Kwa sasa hivi unaweza kumiliki simu nzuri inayokuwezesha
kuingia kwenye mitandao ya kijamii lakini usijue namna ya kuitumia kutengeneza
kipato. Unatumia mtandao wa Facebook, Instagram na WhatsApp lakini hujui
utaitumiaje kutengeneza watu wanaokuamini ili uwauzie bidhaa. Simu yako yaweza
kuwa mtaji, kama una computa nyumbani inaweza kuwa mtaji, kama unakitu chochote
kinachokuunganisha na watu kinaweza kufanyika mtaji.
Power Nguvu)
Wengi
wetu ni vijana tuna nguvu unaweza kujitoa ukafanya kazi za nguvu kwa muda
Fulani hadi ukajitengenezea kiasi cha pesa cha kuanzia biashara. Una uwezo
mkubwa sehemu ipi? Wengine wana vipaji vizuri vya kuongea unawezaji kuongea
vizuri na watu wakawa wateja wako? Wengine wana nguvu ya ushawishi yaani
akiongea na mtu dakika chache wanaweza kuwa marafiki. Unaweza kutumia njia hiyo
pia kama mtaji wako. Utajikusanyia watu ambao unaweza kuja kuwauzia bidhaa
zako.
Time (Muda)
Muda ndio mtaji mkuu nadhani
ningetakiwa niuweke wa kwanza. Unaweza kukosa kila kitu lakini muda utakuwa
nao. Unaweza kuwa huna pesa huna simu, huna chochote lakini una muda.
Unautumiaje muda wako kama mtaji?
Tuseme
wewe ni kijana umemaliza chou na upo nyumbani huna kazi yeyote. Unaweza kutumia
muda ule ulioko nyumbani kujifunza sana kisha ukayatumia hayo unayojifunza kama
katika kubadili Maisha yako.
Inawezekana
wewe unapendelea sana bidhaa tuseme ni mchele. Anza kutafuta watu wanaouza
mchele wa jumla jua mchele gani unauzwa bei gani kwa jumla. Nina rafiki yangu
ananunua mchele Shinyanga gunia la kilo 100 ni Tsh 130 -140(Laki) kwa kawaida
unaweza usiwe na hiyo laki moja ya mtaji wa kununulia huo mchele pia utakosa
mahali pa kuuweka. Unaweza kutafuta wateja 10 tu watakaoweza kununua kilo 10
kila mmoja. Hawa wateja wawe ni watu unaowafahamu na wanaokuamini. Waombe
wakupe pesa za huo mchele tuseme kilo moja ni tsh 2000/= kwa bei ya reja reja.
Kila mteja atatakiwa akupe Tsh 20,000/= kwa kilo kumi. Lakini
ukiangalia kwa bei ya jumla ni Tsh 1300/= hivyo faida yako wewe ni Tsh 700/=
kwenye kila kilo moja au elfu saba kwa kila kilo kumi. Kama utaweza kuupeleka
wote kwa wateja wako hao kumi utakuwa umetengeneza faida ya 70,000/= bila
kuweka pesa yako yeyote. Ukirudia hivyo mara kumi tayari una laki saba. Hapo
huna ofisi wala hujalipa kodi popote. Sana sana utatumia gharama kidogo sana ya
usafirishaji na vifungashio. Ukiongeza idadi ya wateja unaowapelekea tayari
umeshakuwa na biashara kubwa sana inayohitaji ofisi. Ukijiongeza hapo pesa ya
kuanzia biashara unayotaka kuifanya utakuwa umeikamilisha.
Ukimwambia
kijana ajaribu kufanya kitu kama hicho bado atakwambia hawezi au atatoa sababu
zisizoeleweka. Unaweza kuchagua bidhaa yeyote unayoona inahitajika kwenye jamii
unayokaa ukaamua kutumia mfano huo.
Knowledge (Maarifa)
Una maarifa juu ya kitu chochote?
Unaweza kutumia maarifa hayo kama biashara ukatafuta njia ya kuwapa watu na
watu wakulipe. Mfano unaweza kuandika kitabu kinachoelezea kitu unachokifahamu
vizuri. Hapa Kuna mengi sana mfano wake ni vitu ninavyofanya mimi mwenyewe.
People
(Watu)
Unafahamiana
na watu wangapi ambao ukiwaomba pesa wanaweza kukupatia? Kama unao hao watu
nakusihi usiende kuwaomba hela. Tumia mfano niliokupa hapo juu wa mchele uone
ni bidhaa gani unaweza kuwapelekea wakakupa pesa.
Kuna
kipindi nilipata nafasi ya kutembelea maduka ya simu hapa mjini Arusha kwa siku
kadhaa nikajenga mahusiano mazuri na wauza maduka wale. Hivyo nikipita nawapa
salamu. Sasa juzi nikapita madukani mwao nikiwanonyesha njia bora ya kuwasaidia
waweze kufanya mauzo vizuri bila kupoteza mahesabu. Kwasababu tu nilikua
nawafahamu kabla wakanielewa vyema sana. Tukabadilisha na namba za simu ili
kuja kufanya biashara baadae. Ila kuna sehemu nilipita sikuwahi kupita mwanzo.
Ukweli watu wale walikuwa wagumu kunielewa. Nilichojifunza hapo ni kwamba watu
wanapenda kufanya biashara na watu wanaowafahamu na kuwaamini. Wakati huu
unaofikiri huna cha kufanya endelea kujenga uaminifu na mahusiano na watu
mbalimbali. Kuna wakati utafika unatakiwa kuuza bidhaa au kutoa huduma Fulani
iwe ni ajira au umejiajiri lakini ukafanya kwa urahisi sana kwasababu una watu
ambao wanakuamini. Watu ni mtaji unawatumiaje?
Unapokutana
na mtu mpya wewe unamchukuliaje? Binti umekutana na mwanaume anakuomba namba
wakati mwingine huna haja ya kumnyima mpe halafu tafuta kitu cha kuja kumuuzia
lakini sio mwili wako.
Technology
(Teknolojia)
Teknolojia
ni mtaji pia. Kwenye teknolojia kuna vitu vingi sana unaweza kuvitumia kama
mtaji wako. Je unajua namba au group ulizopo Facebook na Wasap unaweza kutumia
kama sehemu ya kuonyesha unachokifanya na ukapata wateja? Je unafahamu simu
yako ni Mtaji? Unaweza kuendesha biashara kwa kutumia simu ya mkononi
(Smartphone). Kwenye teknolojia kuna mambo mengi ambayo tunaweza kuanza
kuchambua moja moja kama somo kabisa. Jinsi ya kutumia blog kibiashara pamoja
na mitandao ya kijamii.
Leo
ninaishia hapa kama bado hujapata mwangaza juu ya mtaji tafadhali wasiliana
nami kwa ushauri Zaidi. Kuna vitu ukinieleza ndio naweza kukupa ushauri
kulingana na mazingira uliyopo na watu waliokuzunguka.
Mwaka
2017 ni mwaka wa Kupiga hatua utoke hapo ulipokuwa.
Jacob Mushi
Entrepreneur
& Author
Arusha
Tanzania.
Fursa nzuri sana kwetu vijana, tujifunze kupitia humu ndan, thank u brother nimepta maarifa mengi mnoo
ReplyDelete