VIJANA NI TUNU YA TAIFA LOLOTE DUNIA
TAIFA lolote Duniani haliwezi kukua
na kuwa imara kiuchumi na kijamii bila makundi yote ya jamii kushirikishwa
kikamilifu katika mapambano dhidi ya umasikini,maradhi na ujinga.
Ni wazi kuwa katika ulimwengu huu wa
sasa,asilimia kubwa ni vijana ambao kimsingi ndio wanaopaswa kuwa viongozi wa
leo na kesho na nguvu yao inahitajika sana katika jamii zetu kutokana na
maarifa na mchango wao katika kusukuma gurudumu la maendeleo ulivyo mkubwa.
Hivyo basi, vijana ni kundi kubwa na
rasilimali muhimu katika kuleta maendeleo ya taifa lolote lile duniani kutokana
na nguvu na fikra za kimapinduzi walizo nazo.
Ukweli wa jambo hilo huwa ni rahisi
kudhihirika waziwazi endapo vijana wataandaliwa vyema katika jamii zao
kushiriki na kushirikishwa katika kubuni, kupanga na kutekeleza mikakati
mbalimbali ya mandeleo.
Viongozi wengi wamekuwa wakisema
mara kwa mara hasa wanapowapa nasaha utasikia wakisikika wakisema “Vijana ni
Taifa la kesho fanyeni kazi kwa bidii na sio kuzurula ovyo, hampaswi kuishi
lelemama na kuzubaa katika vijiwe huku mkipiga soga ambazo hazina umuhimu
katika maisha yenu kwa kuwa kuwepo kwa vijiwe husababisha vishawishi vikubwa
katika anasa na tamaa za kumiliki mali pasipo kufanya kazi.
Kitendo cha kuwafungua vijana
masikio na kuyeyusha fikra mgando ambazo zinatawaliwa na uvivu,uchu wa mali na
maisha ya anasa kilikuwa ni kizuri na chenye busara katika fikra yakinifu
katika kukabiliana na changamoto zao
Ufanyaji wa shughuli za kimaendeleo
ambazo zinaleta ukombozi katika jamii zetu ni jambo la kheri na huleta faraja
katika maisha na mustakabali wa harakati za vijana wenyewe na jamii zao.
Nimekusudia kuandika makala haya
kutokana na kushindwa kuivumilia falsafa inayotumika mara nyingi hasa na
viongozi wengi ambao wanadhamana mbalimbali katika nchi hii,ujumbe unaotolewa
huenda ulikuwa mzuri katika maisha ya vijana lakini kauli ya kusema vijana ni
taifa la kesho ndiyo inayoleta ugomvi katika harakati za vijana na hapa ndio
hoja yangu.
Ni dhahiri kuwa falsafa ya “vijana
Taifa la kesho” imekuwa ikisemwa mara nyingi ambayo ni upotoshwaji mkubwa
katika uhalisia wa mambo licha ya kuwa kauli yenyewe sio ngeni katika masikio
ya jamii, kwani imekuwa ikijirudia mara kwa mara katika majukwaa mbalimbali.
Kuna juhudi kadha wa kadha
zimefanyika na wanaharakati mbalimbali wa masuala ya vijana katika kuipinga
falsafa hiyo na kuonyesha falsafa mbadala katika kuweka mambo sawa na kupunguza
malumbano yasiyo ya msingi
Ila kutokana na ugumu wa wanasiasa
wengi kukubali mabadiliko chanya na yenye kueleweka katika maisha ya vijana kwa
sababu zao binafsi ikiwemo hofu ya kizazi kipya kuchukua nafasi katika nyanja
mbalimbali za uongozi,wanaendelea kuleta mikaganyiko katika jamii kwa faida zao
za ulafi wa madaraka
Viongozi hao wamebaki kutoa mahubiri
hasi ambayo hayana mantiki bali ni nguvu ya kuwavesha vijana kilemba cha ukoka
na fikra mgando za kusubiri muda wa kuitumikia nchi yao kwa kutumia hoja hafifu
ya kjana Taifa la kesho pasipo kesho kutimia
Lugha wanayoitumia ni laghai na kimantiki neno
kesho huwa halikamiliki katika mfululizo wa siku ingawa kimsingi kesho ni neno
ambalo lina uhalisia wake kinadharia zaidi kuliko kivitendo.
Jambo ambalo linathibitishwa na kamusi ya
Kiswahili sanifu iliyotungwa na Taasisi ya uchunguzi wa Kiswahili chuo kikuu
cha Dar-es-salaam ambapo inafafanua kuwa kesho ni “siku inayofuata baada ya
leo, ni wakati ujao”.
Hiyo ina maana kuwa hakuna siku
itimiayo katika mawazo ya kawaida ya binadamu iitwayo kesho kwa kuwa kesho huwa
haifiki, ni siku ambayo inapaswa kusubiriwa tu kila kunapokucha.
Napata tabu sana katika kufikiri ili
nielewe katika tafsiri ya kijana taifa la kesho,sielewi mwanzilishi wa falsafa
hiyo alikuwa anamaanisha nini na kwa maslahi ya nani? Endapo yupo basi nahitaji
mjadala naye ili kuweka sawa hoja husika
Wengi katika jamii waliisikia
falsafa hii kwa mara ya kwanza katika utoto wao na hasa walipokuwa katika
madarasa ya watoto kwenye shule za awali au za msingi.
Ni wazi kuwa walimu walisikika
mashuleni wakiitumia falsafa hii ili kutufanya tujifunze kwa maarifa na ujuzi
na tuzoee kutenda mema na kujijengea sifa nzuri kwa ahadi kuwa sisi ni viongozi
wa baadaye yaani tafsiri nzuri ni “Taifa la kesho”.
Je inawezekana kauli hiyo ilikuwa
sahihi kipindi cha utoto wetu,sisi ambao kwa sasa ni vijana? naamini kila mmoja
kwa kutumia vigezo vyake anaweza kujibu swali hilo hapo juu,
Katika mikataba na sheria mbalimbali
za kimataifa zinafafanua kuwa binadamu mwenye umri kuanzia miaka 0-17 ni mtoto
na haruhusiwi kufanya maamuzi yeyote mazito kuhusu maisha yake, ingawa kamusi
tajwa hapo mwanzo inaleta utata katika vipande viwili vya umri hasa katika
maana ya kijana,kamusi inasema kijana ni mwana mdogo,mtoto mwenye umri wa miaka
7 hadi12.
Lakini katika mtazamo wa kawaida tunaamini
kuwa kijana ni binadamu mwenye umri wa
kuanzia miaka 18-40 na wakati
mwingine mpaka miaka 45.
Ukirejea kamusi tajwa hapo juu tafsiri ya
Taifa ni jamii ya watu wanaoishi katika Nchi moja na wanaounganika kutokana na
matukio ya kihistoria,mfumo wa uchumi na utamaduni chini ya serikali moja.
Kauli ya kijana ni taifa la kesho
kwa namna yoyote ile imepotoshwa kwa mujibu wa tafsiri ya kamusi kuhusu
taifa.Nasema hivyo kwa sababu tunapozungumzia kesho kimantiki ni wakati ambao
unasubiriwa,hata ukizungumza juu ya taifa huwezi kukwepa kutaja
ardhi,mipaka,watu na serikali yao kama vielelezo vya taifa husika,sasa
itakuwaje kijana ambaye yupo useme ni taifa la kesho,rejea tafsiri ya taifa na
kesho
Tafsiri ya mtu kama kijenzi
kimojawapo katika taifa haitugawi katika makundi ya umri wala kabila,awe
mtoto,kijana,mzee,kilema ama vyovyote vile bado mtu atabaki kuwa ni sehemu ya
Taifa tena la leo sio kesho
Pasipo kujali dhana ya wakati
uwe uliopita,uliopo au ujao bali kwa kuzingatia kipindi chote ambacho binadamu
yupo hai.
Naamini huhitaji nguvu nyingi ili
uweze kubaini upotoshwaji uliopo katika falsafa ya kijana ni taifa la kesho kwa
kuwa inapoteza maana ya kijana na juhudi zake katika kufikiri,kubuni na
kuthubutu kutenda.
Kimsingi falsafa hii ina walakini
katika kuichanganua na kuelewa kusudio la mwanzilishi wa falsafa hii kwa kuwa
watu wengi katika mtazamo wao mara wasikiopo neno kijana,humaanisha ni mtu
mwenye umri wa miaka 18 hadi 40 sasa mtu huyo atakuwaje taifa la kesho wakati
yupo leo
Binadamu siku zote tunapaswa kuwa
makini katika fikra zetu na kauli tuzitoazo kwani uzoefu unaonyesha kuwa ndizo
zinazozaa matendo yetu.
Lakini ni muhimu zaidi kusoma
matendo yetu na kuyaelewa kwani matendo tuyatendayo ndiyo hasa tabia zetu.
Natambua pasipo shaka utofauti
uliopo kutoka binadamu mmoja na mwingine katika jamii zetu,juu ya uwezo wa
kufikiri na kuchambua mambo kutokana na sababu za kibailojia.
Hivyo naamini kuwa wapo watu wenye
mtazamo wa kuwaona vijana ni taifa la kesho,binafsi naona mtazamo huo ni
potofu,asiye amini kauli na mtazamo wangu basi mlango upo wazi hivyo karibu
katika mjadala ili kuweka mambo sawa.
Kwa kutumia akili ya kawaida haitamuwia vigumu
binadamu yeyote yule kuona,kushawishika na kukubali mchango wa vijana katika
maendeleo na ustawi wa jamii katika taifa lolote lile.
Kwa kuwa vijana ndio wajenzi wazuri wa taifa
hata hoja kulingana na mazingira stahiki,na wao ndio wanaopaswa kufanya
shughuli zote za kimaendeleo ambapoa wazee wanapaswa kuwa washauri na kuwaachia
vijana nafasi ili waweze kulitumikia taifa lao
Ni wazi kuwa endapo vijana wakipewa
nafasi ya kushiriki katika kuunda taifa na kushughulikia mambo ya kimaendeleo
kama vile ulinzi na usalama,biashara ndogo ndogo na
kubwa,udaktari,ukulima,masuala ya michezo,sheria na mengineyo taifa litapiga
hatua zaidi kimaendeleo.
Kwa misingi hiyo,falsafa ya
kumwona kijana ni taifa la kesho itanapaswa kufa iwe yenyewe au kwa kuiua kwani
bila shaka falsafa hiyo inapaswa kuwa ni taifa la wakati wa sasa wafanyapo kazi
za kujenga taifa lao (Taifa la leo),hivyo itakuwa ni vigumu kuwahadaa vijana
kusubiri taifa la kesho wakati wao wanaishi leo
Falsafa ya vijana ni taifa la kesho
ina ukakasi sana kwa sababu inawejengea vijana tabia ya kusubiri katika
kuchukua hatua juu ya maisha yao.Hivyo inawapa na kuwajengea matumaini ya kuwa
wajinga na wanyonge sambamba na kuhimizwa kuwa na subira kwa vitu
visivyokuwepo.
Ni wazi kuwa muda umefika wa kumwona
kijana ni taifa la leo,sasa hii ndio inapaswa kuwa kauli au falsafa mbadala
kuliko kuiendekeza falsafa ambayo haieleweki katika akili za watu
Katika karne hii ambapo maendeleo ya
sayansi na teknolojia yamesambaa duniani kote vijana wanapaswa kushika madaraka
mbalimbali katika taifa lao,ni jambo la aibu kumkuta mzee ambaye kimsingi
anapaswa kuwa amestaafu bado yupo kazini,huu ni ubinafsi,uchoyo na
ulafi.Inashangaza kuona wazee wakipunguza umri wa kuzaliwa na kuongeza umri wa
kustaafu ili waendelee kung’ang’ania madaraka
Vijana tuamke tuseme ukweli dhidi ya
wazee wetu,wang’atuke na watupishe ili nasi tutimize wajibu wetu,hakuna ulazima
wowote wa wao kuendelea kuzeekea katika madaraka ili hali wana watoto ambao
kimsingi wana elimu ,hali kufikiri,kubuni na kuumba vitu anuai,wazee pumzikeni
kwani wajibu wenu tayari mmeutimiza ulio baki ni wetu vijana.
Comments
Post a Comment