VIJANA NA UCHUMI
Vijana,vijana,vijanaaaaaaa ndio imekua
mada moto sana katika vichwa vya watu wengi sana hapa Tanzania na Duniani kwa
ujumla.Lakini imekua tofauti miongoni mwao kwani wapo baadhi waliojitambua ya
kuwa wao ni vijana na wanatakiwa wafanye nini,ila wapo ambao wametambua wao ni
vijana na wameshindwa kujua wafanye nini,wengine kwa makusudi kabisa na kubaki
kuwalalamikia wazazi na serikali kwa ujumla ya kuwa wamewatenga.
Je,kijana ni nani?ni mtu ambaye yupo
kati ya miaka 15 mpaka 35,kwa mujibu wa malengo ya maendeleo endelevu toka
umoja wa mataifa,wanasema karibia nusu ya idadi ya watu duniani wapo chini ya
miaka 25,manake vijana tunaendelea kuwa wengi duniani.
Lakini hiyo haitoshi,90% ya watu ambao
wapo chini ya miaka 25 wanatoka kwenye nchi zinazoendelea na Tanzania tukiwa
miongoni mwao.pia zaidi ya 67% ya watanzania wote ni vijana hii ni kwa mujibu
wa sense ya mwaka 2012.Hii naweza sema kuwa sisi vijana ni rasilimali kubwa
inayotegemewa na taifa letu lakini na dunia kwa ujumla.
Vijana tumekua watu wa maongezi na
wapangaji mikakati mingi pasipo kuitekeleza kwa vitendo na hivyo kupelekea
kupishana na fursa nyingi zinazojitokeza kwa vijana katika ulimwengu huu ambao
kila kona kijana amekua ni mada kuu katika mazungumzo.
Vijana tumekua watu wa matumizi mengi
kuliko hata vile tunavyoingiza kama kipato,inafikia hatua mpaka mtu anakopa kwa
ajili ya kufanya anasa na starehe zingine za dunia,tumeshindwa kuwa na mikakati
endelevu ya kufanya uzalishaji ili tuweze kulisongesha taifa letu mbele na
badala yake kutumbukia kwenye dimbwi la starehe tu na kushindwa kuwaza,kubuni
na kufanya vitu vya msingi.
Kutokana na ukweli huo,vijana
tunatakiwa kuwa wepesi wa kujifunza na kufanya mambo kwa uharaka na ubora unaohitajika.Ni
lazima tuwe wabunifu katika masuala mbalimbali ya maendeleo,vijana lazima tuwe
wabunifu katika kutafuta mawazo ya kufanya biashara,uwekezaji,utafutaji wa
masoko.Mfano vijana mnaweza pata mtaji kwa kuwa kwenye kikundi na mkacheza
vikoba au mkaomba mkopo nafuu toka halmashauri husika.
Ni muhimu kuwa wabunifu katika kutafuta
mitaji mbalimbali kwa kuzitambua na kuzitumia rasilimali tulizonazo ili ziweze
kuwa na mnyororo mkubwa wa maendeleo ya taifa letu,lakini ikumbukwe kuwa
ubunifu huu uendani na uwezo wa kukabili changamoto zitakazojitokeza katika
shughuli zetu.
Uchumi na vijana ni namna vijana
tunavyoweza kupambanua uwezo na udhaifu,ujuzi na maarifa ya namna ya kumiliki
uchumi wetu,nchi na dunia kwa ujumla,kwa kuangalia maeneo gani ya uhitaji katika
nchi ili sasa uwekezaji wetu uweze kuwa na tija na endelevu.
Uchumi
ni nini?
Uchumi ni jumla ya kazi au shughuli
ambazo mtu,kikundi cha watu,serikali wanafanya ili kutosheleza mahitaji ya
bidhaa au huduma Fulani katika kijiji,kata,wilaya,mkoa,kanda na nchi kwa
ujumla.
Shughuli hizo zaweza kuwa za uzalishaji
na usambazaji wa bidhaa Fulani,utoaji wa huduma halali ili mradi pesa au mapato
yanapatikana.Kuna maeneo ambayo mimi nayaona ni fursa kwetu vijana kama
tutaweza kuyatilia mkazo na kuyapangia mikakati ya maksudi.maeneo kama kilimo
na viwanda yameonekana kuwa manufaa kwetu.
Serikali yetu imeonesha nia ya dhati ya
kutupeleka kwenye uchumi wa viwanda hasa ukiangalia kwenye bajeti ya mwaka huu
2016/17, kwani inakadiriwa zaidi ya 40% imetengwa kwa ajili ya maendeleo
hususani katika ya sekta ya nishati na madini hii inamaana kutakuwepo na
mapinduzi ya umeme na kupelekea sekta ya kilimo na viwanda kuwa na tija.
Ni lazima vijana tuanze kuwekeza katika
viwanda vidogovidogo hususani katika usindikaji wa mazao yatokanayo na kilimo,hii
itatupelekea kuongeza thamani mazao hayo na hivyo kutoa ajira kwa makundi
mengine yanayojishughulisha na kwani masoko yatakua yamepanuka kwa upande wao.
Mfano baada ya serikali kuonesha nia ya
ujenzi wa kiwanda cha kusindika zao la muhogo mkoani lindi kinachokadiriwa
kugharimu zaidi ya billion 1.3 za kitanzania,vijana wengi baada ya kuelimishwa
wameanza kujiingiza katika kilimo cha muhogo ambacho baada ya muda mfupi itakua
lulu kwa maendeleo yao.
Vile vile vijana lazima tuwe na maono
ya mbele katika masuala mbalimbali ya kiuchumi,nakuna kuna kikundi cha vijana
mkoani lindi pia kinaitwa Zinduka kinahamasisha jamii juu ya ufugaji wa kuku na
wanyama wengine,lakini wao wanamalengo ya kuanzisha mashine ya kukoboa na
kusaka nafaka,lakini pia utengenezaji wa chakula cha wanyama.
Hii yote ni kuwa baada ya uhamasishaji
kwa jamii juu ya ufugaji,wao watanufaika kutokana na ongezeko na uhitaji wa
chakula cha mifugo hiyo.hii kuonesha tu kwamba ubunifu na maono ni silaha pekee
ambayo itatutoa kutoka kwenye dimbwi la umasikini tulionao.
Kwa kifupi ni kwamba vijana tutakua
tumeshiriki moja kwa moja katika kukuza uchumi wetu hii ni kutokana na sababu
zifuatazo;
Moja,tutakua tumeongeza pato la taifa
hii ni kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa sokoni ambazo zitatakiwa
kusajiliwa na kuanza kulipa kodi.Lakini pia tutauza bidhaa nje ya nchi na hivyo
kuongeza wigo wa soko letu kutokana na bidhaa zilizofungwa vizuri na zenye
ubora baada ya kupata mafunzo mbalimbali.
Pili, tutakua tumepunguza tatizo la
ajira kwa vijana wenzetu kwani viwanda na mashamba ambayo tutakua tumewekeza
tunatarajia watu watakua wameajiriwa huko.
Tatu,Tutakua tumepunguza mfumuko wa bei
unaotokana na kuingiza bidhaa nyingi toka nchi nyingine,hii ni kutokana na kuongeza
uuzaji wa bidhaa nje ya nchi(exportation) na kupunguza uingizaji wa bidhaa
ambazo tunauwezo wa kuzalisha wenyewe hivyo kupunguza bei ya bidhaa kuwa kubwa
nchini(import inflation).
La mwisho,tutakua sehemu ya kuifanya
shilingi yetu iwe imara kwa kuongeza fedha za kigeni nchini kutokana na uuzaji
wa bidhaa nje ya nchi.
Hivyo basi nchi yoyote duniani ili
iendelee ni lazima ianze na rasilimali watu ambao wengi ni vijana,na lazima
sisi tushirikiane na serikali tuwe mstari wa mbele kuongeza uzalishaji wenye
tija mana ndio tuna nguvu kushinda makundi mengine ya umri.
Ni lazima tuwekeze nguvu katika
kutafuta maarifa ili yatujenge na kutusaidia katika maisha yetu ya kila siku,tusiwe
vijana wa kulalamika tu,tuwe vijana wa kufanya kazi kwanza,vijana ni muhimu
kuwa na ndoto,mikakati ya kuzifikia ndoto zetu,huwezi kupanda bangi na
ukategemea kuvuna mpunga .
Ni wajibu kujua kwamba,kabla hujamlaumu
kiongozi wako,mzazi wako ya kwamba hajakufanyia kitu,jaribu kujiuliza wewe hiyo
elimu yako,nguvu zako,uzuri wako umeifanyia nini jamii inayokuzunguka hata kwa
ushauri tuu.
Vijana lazima tuwe mabalozi wa
maendeleo kwani tuna nguvu na uwezo wa kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja,maarifa
na ujuzi tulionao ni tunu kwa taifa letu hivyo hatuna budi kutumia katika
misingi ya uadilifu na unyenyekevu kwa maendeleo yetu na taifa kwa ujumla
NIMALIZE KWA KUSEMA
HUWEZI KUBADILISHA MAMBO, KWA KUPAMBANA
NA UKWELI ULIOPO.
FILBERT NYONI
MSHAURI MASUALA YA UCHUMI NA
UJASIRIAMALI
MSHAURI MASUALA YA MIRADI YA
KIMAENDELEO NA USIMAMIZI WAKE
MJASIRIAMALI CHIPUKIZI
MWEZESHAJI BIASHARA-MRADI WA ELIMU
FURSA, LINDI
Comments
Post a Comment